Wadau wa Kilimo waishauri Serikali kutambua mfumo usio rasmi wa mbegu

Wadau wa kilimo Mkoani Morogoro wameishauri Serikali kutambua mfumo usio rasmi wa mbegu ili kuendelea  kutunza mbegu za asili kwani inasadikiwa kuwa mfumo huu unachagia zaidi ya asilimia 70 ya mbegu nchini.

Akiwasilisha mada juu ya mfumo wa mbegu unaosimamiwa na wakulima kwenye mafunzo ya uzalishaji mbegu yaliyoandaliwa na Shirika la PELUM Tanzania kupitia mradi wa “mbegu zetu Haki zetu” kwa ufadhili wa Bread for the World, Abdallah Mkindi  Mratibu toka Shirika la TABIO alisema, upo ulazima kwa Serikali  kuupa kipaumbele mfumo huu wa mbegu usio rasmi na hasa kwa kuingiza kipengele katika sheria kitakachotambua mfumo huu.

“Mfumo huu wa mbegu usio rasmi unasadikiwa kutumiwa na wananchi zaidi ya asilimia 70 kote nchini hivyo basi Serikali inapaswa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kilimo kuendeleza mfumo huu kuanzia hatua ya uchaguzi wa mbegu, uhifadhi pamoja na kufanya tafiti shirikishi.”

Mbali na kusisitiza uanzishwaji na uimarishwaji wa benki za mbegu na hasa zile zinazopotea, Mkindi aliongeza kuwa Serikali inapaswa kufanya utafiti wa mbegu asili zote zilizopo, zinazopotea na zilizopotea na kuweza kuzirudisha.

Vilevile Serikali iwe na ushirikiano wa karibu na kituo cha uhifadhi wa nasaba za mimea (National Plant Genetic resources Center) ili kujua nasaba zilizohifadhiwa katika kituo hicho na namna zinavyoweza kuwafikia wakulima pale zinapohitajika.

Mkindi alisema kuwa, kinachozuia  hivi sasa Serikali kutokuunga mkono mfumo huu wa mbegu usio rasmi ni kuamini kuwa mfumo huu ni tishio kwa mfumo rasmi wa mbegu jambo ambalo litapelekea makampuni mengi ya mbegu kufa baada ya wananchi kuacha kununua mbegu hizo na serikali kukosa mapato.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Gaudens Masebe Afisa kilimo toka Kituo cha Kilimo LAELA Rukwa,  alisema mfumo usio rasmi wa mbegu wa ajili ya kilimo endelevu unapaswa kuwa sehemu ya elimu kuanzia mashuleni na hata vyuoni kwani moja ya faida ya mbegu hizi ni kuwa zinakabaliana na mazingira anayotoka mkulima na ni rahisi kuhifadhi kwa njia za asili zisizo na gharama na zinazopatikana kwa urahisi kwenye mazingira ya mkulima eneo lolote

Herman Hishamu Meneja Miradi toka Shirika la Island of Peace Arusha alisema mbegu toka mfumo ulio rasmi zimekuwa na changamoto nyingi kwa wakulima ikiwemo kutokuwepo na uhakika wa mbegu hizo kuota jambo ambalo kila mwaka mkulima anabadili mbegu kwenye shamba moja akitafuta ipi itakuwa na mazao mengi kulingana na sifa wanazopewa.

Akizungumzia upande wa gharama alisema “Mbegu za mfumo rasmi zinauzwa kuanzia shilingi 6000 kwa kilo moja na hivyo kama mkulima atalima hekari moja atapaswa kununua mbegu za shilingi 60,000 jambo ambalo wakulima wengi hawawezi kumudu wakati huohuo anakuja kuuza kilo moja kwa shilingi 400 ambapo atapaswa kuuza kg 15 za mahindi kurudisha shilingi 6000 aliyonunua kilo moja ya mbegu.”

Vilevile alibainisha changamoto nyingine ambazo wakulima wanazipata wanapotumia mfumo rasmi wa mbegu kuwa, mbali na mkulima kununua mbegu, bado atapaswa kununua mbolea kuweka shambani na pia madawa ya kwa ajili ya kuulia wadudu na kuzuia magonjwa.

Francis Mwitumba Meneja Programu toka Shirika la Caritas Mbeya alibainisha kuwa mfumo wa mbegu usio rasmi unamshirikisha moja kwa moja mkulima toka eneo husika hatua zote za uzalishaji mbegu kupitia mazingira anayoishi, uchaguzi na uhifadhi wa mbegu wa hizo huku akiwa na uhakika wa kupata mbegu kwa wakati husika na kwa bei nafuu.

Vilevile alisema mfumo huu wa mbegu unajali pia mbegu za jamii ya mikunde ambayo pia imekuwa msaada mkubwa sana kwa jamii ya watanzania kama vile maharage, karanga, kunde, njugu, choroko, soya, fiwi na mbaazi tofauti na mfumo rasmi wa mbegu ambao unaangalia sana zao la mahindi pamoja na mbogamboga.

Mbali na kutolea mfano wa wakulima toka  kijiji cha Muvwa …ambao baada ya kuanza kutunza na kutumia mbegu zao za maharage, kwa sasa wanavuna jumla ya gunia 4-6 za maharage kwenye hekari moja tofauti na awali ambapo walikuwa wanavuna debe sita kwa hekari moja huku ikiwasaidia pia kukopeshana mbegu na kulipana baada ya kuvuna na kuuza na wakati huohuo kupanda mbegu hizo kwa msimu mwingine tena tofauti na mbegu za kwenye makampuni.

Mradi huu wa  “Mbegu zetu Haki zetu” unaotekelezwa na Shirika la PELUM Tanzania kupitia Masharika wanachama 20 toka Mikoa 13 na kuisha mwaka 2020. Unasisistiza juu ya mfumo usio rasmi wa mbegu  ambapo kaya 400 (wakulima)toka mashirika wanachama wanatarajiwa kunufaika mojamoja na mradi huu.

 

 

 

Our Vision

Prosperous smallholder farmers deriving livelihoods from ecological agriculture

Our Mission

To strengthen capacity of Member Organizations in ecological agriculture for improved smallholder farmers’ livelihood

Our Core Values

  • Accountability
  • Transparency
  • Integrity