Serikali Wilayani Ileje yatambua mchango wa wakulima wazalishaji mbegu

Serikali wilayani Ileje imetambua mchango na jitihada zinazofanywa na wakulima wadogo toka vikundi vya amkeni Msiha na sogea ntembo kwa kuzalisha mbegu ya mahindi ya daraja la kuzimiwa ubora (QDS) aina ya situka ambayo kwa sasa zimeanza kutumiwa na wakulima wengi toka kata ya  Chitete.

Hayo yalibainishwa na Herman Njeje Afisa Kilimo umwagiliaji na Ushurika toka Halmashauri ya Ileje ambapo alisema uwepo wa wazalishaji hao wa mbegu wamekuwa chachu ya mafanikio kwa kundi kubwa la wakulima wilayani Ileje kwani uhitaji wa mbegu hizo umekuwa mkubwa sana na bado haijatosheleza wakulima wa eneo husika.

Alisema pia, kuwepo kwa vikundi hivyo ambavyo vimeweka alama ya kipekee Ileje kupitia uzalishaji huo umewafanya wao kama Halmashauri kuwa na uhakika wa mbegu na kwa wakati muafaka jambo linalosaidia kudhibiti uingizwaji ama ununuzi wa mbegu feki wasizofahamu zilipotoka halikadhalika kudhibiti uchelewashwaji wa mbegu kipindi cha kilimo kwani Halmashauri kupitia wataalamu wake wa kilimo na mbegu wamekuwa wakifuatilia vikundi hivyo tangu uandaaji wa shamba hadi wakati wa kuzifungasha

Aliongeza pia kutokana na juhudi hizo za uzalishaji mbegu. Halmashauri ya Wilaya ya Ileje kupitia wataalamu wake wa kilimo wameendelea kuwa karibu na wakulima hao katika kuhakikisha hawakwami njiani kuanzia kwenye uaandaaji wa shamba la mbegu hadi kufungasha mbegu.

“Wakulima hawa wameonyesha juhudi kubwa na za kipekee katika kuhakikisha uzalishaji wa mbegu hii ya maindi aina ya situka unakuwa endelevu hivyo basi sisi kama Halmashauri tumeamua kutoa kiasi cha fedha zinazotosha kununua hekari mbili za ardhi na wao wameongeza hekari moja kama njia mojawapo ya kuwaongezea eneo la uzalishaji wa mbegu toka robo tatu heka walizokuwa nazo awali na hii ni baada ya kuona kuna uhitaji mkubwa wa mbegu hizi kwa jamii inayowazunguka wakulima hawa,”

Mbali na kuwaongezea hekari hizo za kuzalishia mbegu, halmashauri imekua ikiwapeleka pia kwenye maonyesho  mbalimbali kama njia ya wao kujitangaza na kuendelea kuuza mbegu hizo. Halikadhalika wamekuwa wakitoa msaada wa haraka wa kitaalamu pale inapohitajika na hata kuwaunganisha na wataalamu wa mbegu toka TOSCI pamoja na wataalamu toka SIDO kwa ajili ya upatikanaji wa vifungashio.

Kwa upande wake Sinda Gasheka Mratibu anaosimamia mradi huu wa uhakika wa mbegu kwa uhakika wa chakula na kipato toka shirika la Intergrated Rural Development Organization (IRDO-Ileje) unaotekelezwa na kusimamiwa shirika la PELUM Tanzania kwenye mikoa kumi nchini amesema mbegu hii inayozozalishwa na wanavikundi hawa imekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wengi toka kata ya Chitete wilayani Ileje kutokana na kuleta mavuno mengi.

Mmoja wa wakulima wazalishaji wa mbegu hiyo ya mahindi aina ya situka Maison Siwale alisema mbali na kuwa mbegu hii imeonyesha uzalishaji mzuri jambo linalochangia wakulima wengi kuwa na uhitaji nayo tofauti na mbegu za asili. Lakini inastahimili hali ya hewa pia inawahi kukomaa mapema hata kama mvua ni chache.

Mbali na kushukuru Shirika la PELUM Tanzania kutekeleza mradi huu wa wa uhakika wa mbegu kwa uhakika wa chakula na kipato kwa kushirikiana na shirika la IRDO-Ileje ikiwemo ukaribu wa wataalamu toka Halmashauri ya Ileje katika kuhakikisha wanaendeleza uzalishaji wa mbegu hii ya mahindi

Aliwashukuru pia wanachama wenzake toka kikundi cha amkeni msiha na sogea ntembo kwa kutumia mafunzo vizuri waliyoyapata toka kwa wataalamu wa TOSCI ambapo mafunzo hayo yamewawezesha kuongeza uzalishaji wa mbegu kwenye eneo dogo na hivyo anaamini kuongezeka kwa hekari hizo itawezesha kuzalisha mbegu zaidi na hivyo kupunguza uhitaji wa mbegu kwa wakulima wengi.

Kwa upande wake meneja miradi wa shirika la PELUM Tanzania Rehema Fidelisi aliishukuru Halmashauri ya Ileje kwa kuwa karibu na wakulima hao na kusema kuwa ushirikano huo utasaidia uendelevu wa vikundi hivyo katika uzalishaji wa mbegu hizo za mahindi aina ya situka hata kama mradi huu wa uhakika wa mbegu kwa uhakika wa chakula na kipato unaofadhiliwa na watu wa Bread for the World utafika mwisho.

 

Our Vision

Prosperous smallholder farmers deriving livelihoods from ecological agriculture

Our Mission

To strengthen capacity of Member Organizations in ecological agriculture for improved smallholder farmers’ livelihood

Our Core Values

  • Accountability
  • Transparency
  • Integrity